Na Sammy Anyona Adawo

 

 Kama walivyosema Offside Trick, ‘Kula kitu cha shirika hairidhi hali yangu,’ leo hii nasadikia hayo mawazo. Iweje leo wanadamu wengine wakawa na ujeuri na ukiritimba wa kunyofoa mali ya umma bila haya? Je? Sisi sote si binadamu chini ya jua? Hii dunia si mbaya, binadamu ndio wabaya. Kinyama hichi cha Ufisadi kinanuka moshi na sharti kitupiliwe mbali kama jongoo na mti wake.

Hawa ndumakuwili wenye kujipenda nafsi zao zaidi, hali ni viongozi wamevuruga mamlaka ya mapato (KRA), wanaagiza magari makubwa kutoka nchi za mbali huku wakilenga kukwepa kodi, wanawazuzusha vijana kwa ahadi ghushi na batili na kwa miradi-hewa kama vile ‘kazi kwa vijana’ wakati wakinawiri wao kama shina la mgomba. Hivi leo hela zilizotengewa waathirika wa mafuriko ya mvua za gharika ya Elnino ziko wapi? Ndio wanaomiliki idara ya polisi na vitengo vilivyomo.

Wao ndio majipu yanayofaa kutumbuliwa kulingana na Rais Magufuli. Mbona wasiige mfano wa Magufuli, ndugu zangu? Magufuli anatumbua majipu Tanzania japo kwa upinzani mkali. Kwa kasi yake, naona Tanzania mpya yenye ajira, viwanda na uchumi imara.
Majipu sugu ambayo hayajatumbuliwa nchini Kenya, licha ya ahadi ya kuzitumbua kwa mujibu wa shirika la Transperency International ni;

Anglo-leasing
Ilidhihirika mnamo 2004, akiwa mamlakani Rais mstaafu Moi na kuenea hadi uogozi wa Rais mstaafu Kibaki. Watuhumiwa wakiwa; aliyekuwa waziri wa Fedha David Mwiraria, Seneta wa  Kisii Chris Obure, Bw. Joseph Magari, Deepak Kimani, wote wenye shtaka la kunyang’anya serikali bilioni 4.4 pamoja na matumizi mabaya ya afisi za umma.

Wizi katika Ubalozi wa Tokyo
Shilingi zaidi ya  bilioni 1.5 zilibadhiriwa katika ununuzi wa jumba la ubalozi wa Kenya nchini Japan. Skendo hii ilitokea mnamo mwaka wa 2010 na kuhusisha wizara ya mambo ya nje na ushauri wa kigeni. Waziri husika, kipindi kile, Moses Wetangula, alistaafishwa kwa lazima ili uchunguzi ufanywe.

Shirika la vijana kwa huduma ya kitaifa (NYS)
Watuhumiwa walaji wakiwa, Josephine Kabura, Peter Mangiti, Ben Gethi, Betty Maina wote  katika wizi wa ngawira, kwa mujibu wa wananchi. Zaidi ya shilingi milioni 791 za wakenya zilizotengewa vijana ziliibwa. Anne Waiguru, waziri wakati huo, alikiri kuwa ndiye mfichuzi mkuu wa sakata licha ya madai anuwai ya utepetevu wizarani. La kutia doa, wenzangu, ni kwamba walipoitwa mbele ya kamati ya uhasibu ya bunge, walidhihirisha kauli kanganya;

* Bw. Mangiti (aliyekuwa katibu mkuu wizarani) alishikilia kauli ya kutojua yaliyojiri kwa miaka tatu alizohudumu wizarani – huyu ni mfanyakazi wa serikali aliyekana kujua habari zozote kuhusu wizi wizarani - jukumu lake kuu kwa umma. Maswali yanayoibuliwa ni je? Mshahara alioupokea, kipindi hicho alikistahiki?
*Josephine Kabura (mfanyabiashara aliyezabuniwa jumla ya Bilioni 1.6 kwa kampuni 20 anazomiliki) – huyu kauli yake ni kuwa kampuni 7 kati ya 20 zilisajiliwa chini ya uangalizi wa Bi. Waiguru na kukabidhiwa yeye. Cha kushangaza ni kuwa Waiguru yuadai hamjui wala hajamwona  Kabura. Shere ya mwaka hii! Wakenya wana kichefuchefu maadamu hawaelewi jinsi gani hali hii itawezekana?
*Anne Waiguru (aliyekuwa waziri) asema, ndiye mfichuzi wa sakata, wakati, wote wizarani walimtambua kwa vitisho na utawala wa kiimla na maamuzi tatanishi. Tafakari kisa cha mbweha kuvalia ngozi ya kondoo.

Wakenya wachagize kwa makelele ya mizimu ya jadi ama wakeshe masjid na makanisani kwa sababu ya ufisadi? Huu wizi lazima ukomeshwe.Yamkini, si yote yalioiva yafaa kuliwa, mengine majipu yanayofaa kutumbuliwa.