Na Sammy Anyona Adawo
 
Ajapo mgeni, mwenyeji huliwazwa. Kauli hii, iliyowatoka kinywani wahenga kama ute ilidhihishwa kwetu mnamo tarehe 13 Julai mwaka huu, pale tulipojaaliwa kupata ujio wa wakongwe waliokolea uanahabari. Alikuwepo Domnic Waballa, Jamila Mohammed na Mohammed Ali wote ambao pamoja na kutuelimisha walituhamasisha na uanahabari halisi. Kwa hiyo karibu nikutie skuli....eenh!


Mabingwa hawa walikubali wito, wakaja kwa heshma na taadhima ya wahadhiri wetu; Bw Musakali, Bw Makori, Bw Omanga na idara mzima ya uanahabari katika chuo kikuu cha Moi.

Domnic Waballa, mwanahabari aliyewahi kufichua biashara ya mihadarati yenye kima cha thamani ya shilingi bilioni 6.4 nchini Kenya, ndiye aliyetanguliza mdahalo. Jagina huyu aliweka dhahiri umuhimu wa uandishi wa makala katika uanahabari. Kulingana naye, hamna msingi wowote unaopiku uandishi wa makala. Anafafanua kuwa anapojihusisha na uandishi wa makala, mwanahabari hupanuka mawazo akawa na uwezo mkuu wa kuwasilisha hoja na kutoa maoni pamoja na udadisi wa mitizamo. La pili ni haki ya usawa wa maoni almaarufu ‘right of reply,’ anakanya tabia ya kutowapa wahusika ama waathirika wa taarifa nafasi ya kuchangia madai juu yao. Tatu ni uhakikisho wa deta unazozipokea, kama mwanahabari hususan kitengo cha upekuzi. Alitusimulia kisa kuhusu uhakikisho wa deta na jinsi alinusurika kifo. Huyu mwanahabari anaongezea kuwa huu uhakikisho unaweza fanyika kwa muda wa wiki moja ama hata mwaka mzima kulingana na uzito wa mada. Ucheshi nao haukumkoma huyu mtaalam alipotustaajabisha kuwa, katika pilikapilika zake za kutafuta habari kwa upekuzi alibugia mvinyo kwa masaa 72 pasi na kuzidiwa chakari.

Jamila Mohammed akawa wa pili kuja. Kama mtangazaji wa runinga, alitupa mwanga kuhusu vigezo vya uanahabari halisi. Mandhari yalikuwa ya busara. Alianza kwa salamu zilizowajaa tabasamu walokuwepo mhadharani. Huyu binti mchangamfu na mwenye furaha alituelekeza kwa utaratibu, hoja moja baada ya nyingine. Ustaarabu wake ulipelekea, mmoja wetu kumuliza kama kuna makadirio fulani yanayoangaziwa katika uteuzi wa watangazaji wa zamu. Mfano; Nimrod Taabu na Jamila. Alikubali kwamba makadirio yapo, akaongeza kuwa wale watangazaji wa zamu sharti wawe na uelewa wa kila mmoja, marafiki na wenye kuaminiana kwa ajili ya mtazamaji. Jamila si mgeni wa utangazaji, hivyo basi ana wafuasi lukuki mitandaoni. Anasema kuwa mtangazaji lazima awe mwadilifu, mjasiri, mmilisi wa lugha na mwenye uwezo wa kushirikiana na kutangamana na wenzake. Alitueleza kuwa maripota sharti waelezee matukio na mandhari ya taarifa zao hasa wanapotutaarifu wakiwa maeneo haya. Maelezo hayo yawe hususan ya hisia, harufu na dhana dhahania - yasiyoweza kuonwa wala kushikwa. Kama ukimhoji mgeni, maswali yawe sahili na yanayoeleweka kwa urahisi. Vile vile ukumbuke kuwa idadi ya meneno yazingatiwe kwa mujibu wa muda uliotengewa kipindi hicho. Mathalani; maneno matatu kwa sekunde.  Jamila ana sisitiza umuhimu wa mwanahabari kuwa na umilisi wa lugha ya  Kiswahili na Kiingereza kama yeye alivyo. Vile vile alitupa mwanga kuhusu mfumo wa kisasa wa Octopus wa kuandaa mwelekezo wa kipindi ama Script.

Mohammed Ali, mhariri mkuu kitengo cha Upekuzi ndiye aliyehitimisha wiki ya uanahabari. Sifa zake zilizotamba humu nchini haziwezi kutiwa doa wala kudra zake kufanyiwa shere. Lahaula! Sauti yake kama mkarara? Ali yuazama na kuibuka na mara afanyavo hivyo, Wakenya hupata mzinduko wa aina yake. Mdahalo ulitangulizwa kwa video yenye kuonyesha uwazi wa mauaji yanayotekelezwa na serikali bila kuzingatia sheria. Alituonyesha hali duni katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City, inayopelekea ushahidi na ithibati kupotezwa kimaksuudi. Ufichuzi wake wa karibu uliweka wazi utepetevu wa idara ya ujasusi nchini Kenya, kupitia upekuzi wa mauaji ya mfanyabiashara Jacob Juma. Katika kazi yake hii ilidhihirika kuwepo kwa kitengo maalum katika idara ya polisi kinachofanya mauaji ya wakenya. Shirika la kitaifa la ujasusi linaloongozwa na Meja-Generali Philip Kameru nalo limetiwa mizani kufuatia madai ya kufichwa kwa habari, kinyume na sheria. Mohammed Ali alituhimiza kuwa na jicho pevu katika kuchunguza matukio. Anasema kwamba shahidi wako, kama mwanahabari ni muhimu asifichuliwe kwa umma na kwamba kusudi la kumfichua liwe tu iwapo maisha yake yamo hatarini. Ali alitukanya na ukabila, vile vile akatushauri kuwa magaidi hawana msingi katika imani yoyote ile na kwamba ukristo haukubali mauaji sawa na uislamu.  

Uanahabari si utanashati wala urembo, uanahabari ni wito wa kujituma kutumikia wanadamu.