Ajapo mgeni, mwenyeji huliwazwa. Kauli hii,
iliyowatoka kinywani wahenga kama ute ilidhihishwa kwetu mnamo tarehe 13
Julai mwaka huu, pale tulipojaaliwa kupata ujio wa wakongwe waliokolea
uanahabari. Alikuwepo Domnic Waballa, Jamila Mohammed na Mohammed Ali wote
ambao pamoja na kutuelimisha walituhamasisha na uanahabari halisi. Kwa hiyo
karibu nikutie skuli....eenh!
Mabingwa hawa walikubali wito, wakaja kwa
heshma na taadhima ya wahadhiri wetu; Bw Musakali, Bw Makori, Bw Omanga na
idara mzima ya uanahabari katika chuo kikuu cha Moi.
Domnic Waballa, mwanahabari aliyewahi kufichua
biashara ya mihadarati yenye kima cha thamani ya shilingi bilioni 6.4 nchini
Kenya, ndiye aliyetanguliza mdahalo. Jagina huyu aliweka dhahiri umuhimu wa
uandishi wa makala katika uanahabari. Kulingana naye, hamna msingi wowote
unaopiku uandishi wa makala. Anafafanua kuwa anapojihusisha na uandishi wa
makala, mwanahabari hupanuka mawazo akawa na uwezo mkuu wa kuwasilisha hoja na
kutoa maoni pamoja na udadisi wa mitizamo. La pili ni haki ya usawa wa maoni
almaarufu ‘right of reply,’ anakanya tabia ya kutowapa wahusika ama waathirika
wa taarifa nafasi ya kuchangia madai juu yao. Tatu ni uhakikisho wa deta unazozipokea,
kama mwanahabari hususan kitengo cha upekuzi. Alitusimulia kisa kuhusu
uhakikisho wa deta na jinsi alinusurika kifo. Huyu mwanahabari anaongezea kuwa
huu uhakikisho unaweza fanyika kwa muda wa wiki moja ama hata mwaka mzima
kulingana na uzito wa mada. Ucheshi nao haukumkoma huyu mtaalam
alipotustaajabisha kuwa, katika pilikapilika zake za kutafuta habari kwa
upekuzi alibugia mvinyo kwa masaa 72 pasi na kuzidiwa chakari.
Jamila Mohammed akawa wa pili kuja. Kama
mtangazaji wa runinga, alitupa mwanga kuhusu vigezo vya uanahabari halisi.
Mandhari yalikuwa ya busara. Alianza kwa salamu zilizowajaa tabasamu walokuwepo
mhadharani. Huyu binti mchangamfu na mwenye furaha alituelekeza kwa utaratibu,
hoja moja baada ya nyingine. Ustaarabu wake ulipelekea, mmoja wetu kumuliza
kama kuna makadirio fulani yanayoangaziwa katika uteuzi wa watangazaji wa zamu.
Mfano; Nimrod Taabu na Jamila. Alikubali kwamba makadirio yapo, akaongeza kuwa
wale watangazaji wa zamu sharti wawe na uelewa wa kila mmoja, marafiki na wenye
kuaminiana kwa ajili ya mtazamaji. Jamila si mgeni wa utangazaji, hivyo basi
ana wafuasi lukuki mitandaoni. Anasema kuwa mtangazaji lazima awe mwadilifu,
mjasiri, mmilisi wa lugha na mwenye uwezo wa kushirikiana na kutangamana na
wenzake. Alitueleza kuwa maripota sharti waelezee matukio na mandhari ya
taarifa zao hasa wanapotutaarifu wakiwa maeneo haya. Maelezo hayo yawe hususan
ya hisia, harufu na dhana dhahania - yasiyoweza kuonwa wala kushikwa. Kama
ukimhoji mgeni, maswali yawe sahili na yanayoeleweka kwa urahisi. Vile vile
ukumbuke kuwa idadi ya meneno yazingatiwe kwa mujibu wa muda uliotengewa
kipindi hicho. Mathalani; maneno matatu kwa sekunde. Jamila ana sisitiza umuhimu wa mwanahabari
kuwa na umilisi wa lugha ya Kiswahili na
Kiingereza kama yeye alivyo. Vile vile alitupa mwanga kuhusu mfumo wa kisasa wa
Octopus wa kuandaa mwelekezo wa kipindi ama Script.
Mohammed Ali, mhariri mkuu kitengo cha Upekuzi
ndiye aliyehitimisha wiki ya uanahabari. Sifa zake zilizotamba humu nchini
haziwezi kutiwa doa wala kudra zake kufanyiwa shere. Lahaula! Sauti yake kama
mkarara? Ali yuazama na kuibuka na mara afanyavo hivyo, Wakenya hupata mzinduko
wa aina yake. Mdahalo ulitangulizwa kwa video yenye kuonyesha uwazi wa mauaji
yanayotekelezwa na serikali bila kuzingatia sheria. Alituonyesha hali duni
katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City, inayopelekea ushahidi na ithibati
kupotezwa kimaksuudi. Ufichuzi wake wa karibu uliweka wazi utepetevu wa idara
ya ujasusi nchini Kenya, kupitia upekuzi wa mauaji ya mfanyabiashara Jacob Juma.
Katika kazi yake hii ilidhihirika kuwepo kwa kitengo maalum katika idara ya
polisi kinachofanya mauaji ya wakenya. Shirika la kitaifa la ujasusi
linaloongozwa na Meja-Generali Philip Kameru nalo limetiwa mizani kufuatia madai ya
kufichwa kwa habari, kinyume na sheria. Mohammed Ali alituhimiza kuwa na jicho
pevu katika kuchunguza matukio. Anasema kwamba shahidi wako, kama mwanahabari
ni muhimu asifichuliwe kwa umma na kwamba kusudi la kumfichua liwe tu iwapo
maisha yake yamo hatarini. Ali alitukanya na ukabila, vile vile akatushauri
kuwa magaidi hawana msingi katika imani yoyote ile na kwamba ukristo haukubali
mauaji sawa na uislamu.
Uanahabari si utanashati wala urembo,
uanahabari ni wito wa kujituma kutumikia wanadamu.
26 Comments
Umeeleza kwa kina tena bila dosari ya aina yoyote. Waliosema wakuu hawa, hayahitililafiani bali yanaingiliana. Ningependa japo kwa udogo kusisitiza aliyoyasema Ndugu Mohammed Ali. Kwa kweli, kazi hii ya uanababari pasi na kufichua maovu ya jamii, inaweza kumtia mwanahabari katika mashaka na hofu ya kupoteza maisha yake. Naamini ni muhimu kwa makada na serikali kuu kushirikiana katika kuhusisha usalama kwa mwanahabari binafsi. Ila nashangaa atakavyopewa usalama huu ikiwa maovu aliyoyafichua huenda yakahusika na serikali. Itakuwa tatizo kutegemea usalama kutoka kwa wale uliowatumbua. Hii ndiyo sababu ya umuhimu wa njia mbadala au usalama usiotegemezi kwa masharti ya serikali kuu. Jopo au kamati ya uanahabari nchini inapaswa kuchunguza mikakati mwafaka ya kuwalinda wanaharakati hawa wanaotia maisha yao hatarini kwa faida ya mwanajamii aliyefumbwa macho. Hili ni jambo la muhimu lisilohitaji kupuuzwa. Halikadhalika, wanafunzi nao wanapaswa kushirikishwa katika warsha za kuwaelimisha kuhusu madhara wanayoweza kukumbana nayo kwenye uanaharakati huu. Itampasa mwanafunzi wa uanahabari kufahamu jinsi sheria ikivyo katika kulinda haki yake ya kuishi na uwepo wa watakaohakikisha inatiwa maanani.
ReplyDeleteNdugu mwanahabari, nimefurahishwa na uliyoyaeleza kuhusu mkutano huu wa hadhara uliohudhuria. Pongezi ziwaendee washikadau waliohusika katika kuifanikisha. Hayo ndiyo niliosutwa na moyo wangu kunena kuhusu haya ya muhimu. Ahsante!
kweli David, ulinzi unafaa, tatizo tu ni kwamba wanaopaswa kuwalinda raia wamewageukia raia
DeleteGood writing.
ReplyDeleteHitimisho nzuri, Uanahabari ni wito!!
Asante nashukuru sana Bett. Ni wito
Deletejagina wa lugha wewe! umeelezea kinagaubaga yaliyotukia. Lugha hii umeimudu kwelikweli
ReplyDeleteYegon rafiki yangu, nina imani siku ipo tutajulikana barani Afrika na kote ulimwenguni kwa lugha hii.
DeleteWell said and highlighted.
ReplyDeleteKuongezea labda,uhanahabari ni kujiamini na Kuwa na kipaumbele.
Asante ndugu yangu Carloz
DeleteNice piece
ReplyDeleteWanahabari huriski sana lakini... Naafikiana na pendekezo lako kwamba Jopo au kamati ya uanahabari yafaa izindue mikakati mwafaka ya kuwalinda wanahabari
kweli kabisa ila inatupasa kujilinda kwa kiasi kikubwa maadamu mambo ya polisi yamekuwa magumu nchini
Deleteuandishi huu ni bora kabisa...uanahabiri ni kujitolea kwa minajili ya jamii na wananchi, na ninawashukuru sana wanahabiri wote wanaojitoleo usiku na mchana kuhakikisha kuwa tunaharifiwa vilivyo.
ReplyDeleteAsante, hatuwezi kuukataa huu wito.
DeleteNice article looking forarad for more of your articles
ReplyDeleteThanks Charles keep it here, I pledge to write some-more
DeleteUandishi safi kaka. Umegonga ndipo.
ReplyDeleteAsante sana Bw. Musakali.
DeleteUandishi safi kaka. Umegonga ndipo.
ReplyDeleteUmenena ukweli kinagaubaga. Kweli kweli uanahabari ni wito
ReplyDeleteKazi nzuri Sana...keep it up
ReplyDeleteHitimisho kali sana kakangu.
ReplyDelete"...Uanahabari si utanashati wala urembo, ni wito wa kujituma kutumikia wanadamu." mwanahabari ni yule ambaye amejitokeza na ambaye ana kipaji cha kutumikia jamii kwa kuwaelimisha na kuwajuza kuhusu yanayotendeka kote duniani, kazi ambayo haiwezi kufanywa na mtu yeyote yule. *Uanahabari ni wito* ����✔
Asante sana Elijah. Ni wito kweli.
DeleteNimeitikia kaka. Sikuweza kuhudhuria siku zote lakini mwangaza umenionyesha. Kiswahili kiko sawa kabisa. Asante kwa makal haya. ENdelea vivyo
ReplyDeleteJanet shukrani za dhati. namshukuru Mola kwa lugha yetu
DeleteNice article looking forarad for more of your articles
ReplyDelete"...Ucheshi nao haukumkoma huyu mtaalam alipotustaajabisha kuwa, katika pilikapilika zake za kutafuta habari kwa upekuzi alibugia mvinyo kwa masaa 72 pasi na kuzidiwa chakari." kweli uanahabari ni wito. Jambo nzito hilo
ReplyDeleteHongera kaka
ReplyDeleteHakika kila ninaposoma vipengele unavyo gusia naona weledi wako katika kitengo hiki cha uandishi na utafiti wa habari unazidi kuimarika mengi umeyasema ya ukweli hakuna dosari kwangu ni heko na kuzidi kutegea makala yako zaidi nipate kujua mengi zaidi Hakika hapa kwako hujifunza mengi tia bidii juu huu ni mwito na ukapata mhakiki kabisa