Confronting Inequity - Participation in Governance.













Confronting Inequity; prticipation in Governance.

Essay Language: Swahili

Mada Kuu: Kuukabili Utovu wa Usawa

Mada: Ushirikisho katika Utawala.

Utangulizi: Wenye hekima husema, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Ili tuwe na Utawala imara, sharti tushirikishe vitengo vyote vya jamii wala pasiwe na upungufu katika juhudi za kuleta usawa.

Kuhusishwa kwa wanahabari katika Utawala.
Wanahabari wametengwa katika maswala ya Utawala. Katika taifa la Kenya, ni wazi kwamba wanahabari wamepata kujeruhiwa na hata kuwawa huku wakiwa katika harakati ya kufichua kashfa ya ufisadi kama vile vitisho alivyopokea Mohamed Ali mwenye kipindi cha mafichuzi maarufu kama Jicho Pevu katika runinga ya KTN (Kenya Television Network) na dhulma za serikali pamoja na mauaji ya raia kinyume na sheria. Uanahabari vile vile hudhalilishwa na seikali pale wanapoangazia taarifa zilizokinyume na matakwa ya wachache serikalini. Kwa mfano, mnamo Januari 30, mwaka wa 2018, serikali ya Kenya iliweza kuzima kwa muda wa siku tatu vyombo vya habari vyote ambavyo vilipeperusha uapisho wa kiongozi wa upinzani Mheshimiwa Raila Odinga kwa madai kwamba vituo vilivyohusika (KTN, KTN NEWS, NTV- Runinga ya Nation, CitizenTV) vilikiuka sheria kipengele kinachohusika na usalama wa taifa. Ikumbukwe kwamba ili kuwe na ufanisi katika Utawala sharti misingi ya democrasia na Uhuru wa Wanahabari izingatiwe. Tawala za kiimla huchangia unyanyapaa wa asasi muhimu uongozini kama vile Uanahabari na Uhuru zinazoendana na kipengele 35 kwa mujibu wa katiba ya Kenya.

Kuhusishwa kwa wanaoishi na ulemavu katika nafasi za uongozi.

Uongozi ni sehemu muhimu ya Utawala. Viongozi katika taifa la Kenya huchaguliwa na wananchi kwa kupigiwa kura kwenye uchaguzi mkuu. Ila panatokea hali ya kutokuwa na uwakilishi kamili hususan ukizingatia jamii ya watu wanaoishi na ulemavu nchini ambao aghalabu hutelekezwa na familia zao wenyewe, uwakilishi huu haujakuwa toshelezi. Nchini Kenya, sheria (kipengele 54) inawapa nafasi maalum watu wanaoishi na ulemavu ili kuzitwaa nyadhifa mbali mbali serikalini bali changamoto kuu ni kwamba sheria zenyewe hazitekelezwi barabara wala hamna anayefuatiliza ili kuhakikisha utekelezi unafanywa. Hivyo kulemaza sheria na watu wanaoishi na ulemavu, ambao wangechangia ujenzi wa uchumi miongoni mwa vitendo vingine vya kujenga taifa.

Ni muhimu kujua ya kwamba changamoto hii inaweza kukabiliwa kwa kuongeza idadi ya wawakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu nchini kupitia uwasilishaji wa mswada bungeni ili kujadiliwa. Vile vile, ni vyema wawe na haki sawa katika nyadhifa za kazi, (kampuni za binafsi na zile za serilkali) sharti kuwe na idadi maalum iliyotengewa watu wenye ulemavu wa namna tofauti tofauti kama vile ulemavu wa ngozi – ambao katika taifa la Kenya na taifa jirani la Tanzania huwindwa na waganga na wachawi ili kupata viungo vyao kwa maswala ya kishirikina. Suluhisho kuu katika Kuukabili ukosefu wa usawa baina ya jamii ya watu wanaoishi na ulemavu na wale wasio na ulemavu utapatikana pale serikali kuu itakapowajibika kuhamasisha umma dhidi ya dhana kama hizo potovu kando na kutunga sheria kali kukabiliana na wanaoshiriki unyanyapaa wa watu wanaoishi na ulemavu.

Kushirikishwa kwa vijana katika maswala ya Utawala.

Njia mojawapo ya kuleta usawa katika taifa ni kuhakikisha kwamba vijana wanahusishwa katika maswala ya Utawala. Nchini Kenya chini ya kipengele 55 katika katiba ya Kenya, tunapata mafungo yanayoshughulikia vijana na mahitaji yao. Miongoni mwa mahitaji yanayoshughulikiwa kwenye sheria hiyo ni pamoja na; nafasi za ajira, kulindwa kutokana na mila inayoweza kuwadhuru na kuelimishwa.

Katika taifa la Kenya vijana wengi wanajihusisha na usanii ama sanaa ya namna fulani. Vijana wanatengeneza shanga, michoro pamoja na tungo za nyimbo ambazo mara kwa mara huwa na jumbe zenye maudhui kama vile utaifa, ukabila, ufisadi, demorasia na mengine ambayo yanaweza yakawa muhimu katika Utawala wa taifa.

Kwa mfano wimbo; “Utawala” wa mwanamuziki, Juliani wenye mkarara unaosema “sitasimama maovu ya kitawala…undugu ni kufaana” umetumika sana na wanaharakati na wakereketwa katika kupigania haki ya wakenya.

Mfano mwingine, unapatikana kwenye wimbo wa mtunzi mashuhuri Eric Wainaina katika wimbo maarufu “nchi ya kitu kidogo” ambao unazungumzia ufisadi ambao unajulikana kama chai ama kitu kidogo nchini Kenya. Wimbo huu unaonya kwamba ufisadi unatisha jamuhuri yetu na ni shuruti tuuondoe kabla utumalize.

Hitimisho: Kwa mtizamo wangu, ujumuisho wa walemavu, vijana, wanawake na wanahabari katika utawala utaleta mafanikio makubwa katika juhudi za kuleta usawa.

Mikakati ninayoshughulikia Kukabili Utovu wa Usawa:

Maishani nimekuwa na azma ya kuwapa sauti wanyonge na waliokandamizwa katika jamii, hivyo nilianza tovuti yangu http://www.sammyanyona.blogspot.com ilimuradi nipate kutoa mchango wangu kuhusu maswala ya siasa na utawala mwema.

Kwenye tovuti yangu naangazia juhudi wanazofanya wanajamii ili kuinua mapato ya vijana pamoja na kukuza talanta nyingi ambazo wanazo. Vile vile, pale kwenye tovuti, nachanganua maswala ya kisiasa na kukashifu viongozi wafisadi.

Post a Comment

0 Comments