KINYAMA KINUKACHO MOSHI - 'Siri Kali Ya Wala Nyama'


Na Sammy Anyona Adawo

 

 Kama walivyosema Offside Trick, ‘Kula kitu cha shirika hairidhi hali yangu,’ leo hii nasadikia hayo mawazo. Iweje leo wanadamu wengine wakawa na ujeuri na ukiritimba wa kunyofoa mali ya umma bila haya? Je? Sisi sote si binadamu chini ya jua? Hii dunia si mbaya, binadamu ndio wabaya. Kinyama hichi cha Ufisadi kinanuka moshi na sharti kitupiliwe mbali kama jongoo na mti wake.

Hawa ndumakuwili wenye kujipenda nafsi zao zaidi, hali ni viongozi wamevuruga mamlaka ya mapato (KRA), wanaagiza magari makubwa kutoka nchi za mbali huku wakilenga kukwepa kodi, wanawazuzusha vijana kwa ahadi ghushi na batili na kwa miradi-hewa kama vile ‘kazi kwa vijana’ wakati wakinawiri wao kama shina la mgomba. Hivi leo hela zilizotengewa waathirika wa mafuriko ya mvua za gharika ya Elnino ziko wapi? Ndio wanaomiliki idara ya polisi na vitengo vilivyomo.

Wao ndio majipu yanayofaa kutumbuliwa kulingana na Rais Magufuli. Mbona wasiige mfano wa Magufuli, ndugu zangu? Magufuli anatumbua majipu Tanzania japo kwa upinzani mkali. Kwa kasi yake, naona Tanzania mpya yenye ajira, viwanda na uchumi imara.
Majipu sugu ambayo hayajatumbuliwa nchini Kenya, licha ya ahadi ya kuzitumbua kwa mujibu wa shirika la Transperency International ni;

Anglo-leasing
Ilidhihirika mnamo 2004, akiwa mamlakani Rais mstaafu Moi na kuenea hadi uogozi wa Rais mstaafu Kibaki. Watuhumiwa wakiwa; aliyekuwa waziri wa Fedha David Mwiraria, Seneta wa  Kisii Chris Obure, Bw. Joseph Magari, Deepak Kimani, wote wenye shtaka la kunyang’anya serikali bilioni 4.4 pamoja na matumizi mabaya ya afisi za umma.

Wizi katika Ubalozi wa Tokyo
Shilingi zaidi ya  bilioni 1.5 zilibadhiriwa katika ununuzi wa jumba la ubalozi wa Kenya nchini Japan. Skendo hii ilitokea mnamo mwaka wa 2010 na kuhusisha wizara ya mambo ya nje na ushauri wa kigeni. Waziri husika, kipindi kile, Moses Wetangula, alistaafishwa kwa lazima ili uchunguzi ufanywe.

Shirika la vijana kwa huduma ya kitaifa (NYS)
Watuhumiwa walaji wakiwa, Josephine Kabura, Peter Mangiti, Ben Gethi, Betty Maina wote  katika wizi wa ngawira, kwa mujibu wa wananchi. Zaidi ya shilingi milioni 791 za wakenya zilizotengewa vijana ziliibwa. Anne Waiguru, waziri wakati huo, alikiri kuwa ndiye mfichuzi mkuu wa sakata licha ya madai anuwai ya utepetevu wizarani. La kutia doa, wenzangu, ni kwamba walipoitwa mbele ya kamati ya uhasibu ya bunge, walidhihirisha kauli kanganya;

* Bw. Mangiti (aliyekuwa katibu mkuu wizarani) alishikilia kauli ya kutojua yaliyojiri kwa miaka tatu alizohudumu wizarani – huyu ni mfanyakazi wa serikali aliyekana kujua habari zozote kuhusu wizi wizarani - jukumu lake kuu kwa umma. Maswali yanayoibuliwa ni je? Mshahara alioupokea, kipindi hicho alikistahiki?
*Josephine Kabura (mfanyabiashara aliyezabuniwa jumla ya Bilioni 1.6 kwa kampuni 20 anazomiliki) – huyu kauli yake ni kuwa kampuni 7 kati ya 20 zilisajiliwa chini ya uangalizi wa Bi. Waiguru na kukabidhiwa yeye. Cha kushangaza ni kuwa Waiguru yuadai hamjui wala hajamwona  Kabura. Shere ya mwaka hii! Wakenya wana kichefuchefu maadamu hawaelewi jinsi gani hali hii itawezekana?
*Anne Waiguru (aliyekuwa waziri) asema, ndiye mfichuzi wa sakata, wakati, wote wizarani walimtambua kwa vitisho na utawala wa kiimla na maamuzi tatanishi. Tafakari kisa cha mbweha kuvalia ngozi ya kondoo.

Wakenya wachagize kwa makelele ya mizimu ya jadi ama wakeshe masjid na makanisani kwa sababu ya ufisadi? Huu wizi lazima ukomeshwe.Yamkini, si yote yalioiva yafaa kuliwa, mengine majipu yanayofaa kutumbuliwa.

Post a Comment

10 Comments

  1. Asante sana kwa hii Habari, ufisadi lazma ishindwe nchi hii

    ReplyDelete
  2. Kweli, James nakuunga mkono. This has become so bad, that if someone actually does what is required of him (Matiang'i) people get amazed beyond their wits

    ReplyDelete
  3. It Is perplexing how Kenyans see corruption as a way of life and have allowed it to become a norm in the society. Disappointed that the people expected to spearhead the fight if this vice are allegedly part of the problem...

    Good piece Sammy

    ReplyDelete
  4. True, it's time we woke up from this mediocrity that creeped into our policy implementation and do things right. Thanks Bonnie

    ReplyDelete
  5. Kwa mtazamo wangu,sisi wenyewe ndio fisadi, hivyo tunawachagua viongozi fisadi kama sisi. Hili linadhihirika tunapohongwa ili kupigia "majipu" haya kura kuwatia uongizini. Hata hivyo, nina matumaini kwamba ipo siku moja ufisadi utakua swala la kutajwa tu, tutauzika katika kaburi la sahau. Shida ni kwamba hii ni historia mbaya inayopaka jina la taifa hili tope.

    ReplyDelete
  6. Ndugu Sammy, maoni yako makali na yanatekeleza haki katika kulikabili adha hii. Siku zote mwasho ndio unaosababisha kujikuna. Hivyo basi, mwasho waliosababishiwa wananchi ndio utaoanza hatua ya kushinikiza mapinduzi na mabadiliko yatakayoleta mageuzi katika matumizi ya rasilimali za serikali. Kuna ubadhirifu mkubwa katika idara nyingi za serikali inayotia wananchi mashaka makubwa.
    @_mugambi254; Nayasidiki unayobashiri kuhusu upotovu wa hali hii katika miaka za baadaye. Ila nahofia kuwa katika mfumo huu mbaya huenda tukaishiwa na rasilimali za kusitiri mustakabali wa jamii ambayo huenda yakaifikia kesho hiyo.
    Tatizo la nchi hii si ukosefu wa miundombinu za kulikabili janga hili bali ukosefu wa watu wa kuaminika katika utekelezaji. Zipo idara za serikali na zisizo za kiserikali ambayo yana wajibu katika kulikosoa serikali, kukomesha ubadhirifu na kuhakikisha haki katika uwajibikaji kwa mwananchi. Japo kinachosikitisha ni kuwa hamna anayefanya kazi yake kama inavyotakikana. Cha kuvunda zaidi ni kuwa hata wanaoteuliwa wanajiuzulu kwa kuhofia maisha yao miongoni mwa sababu nyingine fiche. Imefika hatua wananchi wakawaza kuwa huenda kumteua kiongozi wa dini kulisimamia jopo hili itadiriki japo kuhakikisha kodi za mwananchi zinatumika ipasavyo.
    Naamini mageuzi tunayoyatarajia yatakuwepo kwa muungano wa wananchi kulikabili tatizo hili kwa umoja. Hapawezi pakawa na mabadiliko wananchi wanapotengana. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Hatuwezi tukajikunyata katika nyumba zetu kwa utulivu bila wasiwasi tukiyaona haya. Hatuwezi tukawaacha wachache kupogania haki zetu huku tukija kufurahia katika kile ambacho hatukuhusika. Hivyo, hatutakuwa tofauti na wale wanaofyonza uhai wa nchi yetu. Tusitenge kazi hii kwa wachache. Hili ni jambo linalohitaji huduma yetu sote maadamu wote ni wadau katika serikali hii. Serikali sio walioteuliwa. La, hasha! Kila mmoja wetu ni sehemu, japo ndogo ya serikali tunayoilaumu. Tunatakiwa wote kuwajibika na kuwakosoa wenzetu ikiwemo kutowapa kura wanaotuponza haki yetu kama alivyodokeza Jimmie Bonnie.
    Heko, ndugu mtangazaji kwa kazi bora uliyoifanya katika kutotusahaulisha hivi tunavyovisahau kwa wepesi. Hongera!

    ReplyDelete
  7. Ni jambo la kusikitisha, ila great piece of work

    ReplyDelete